Rulani Mokwena Kuendelea Kuinoa Wydad Casablanca Licha ya Shinikizo

Licha ya presha kubwa kutoka kwa wadau wa klabu wakitaka kocha huyo aondolewe kufuatia matokeo yasiyoridhisha, uongozi umeamua kuendeleza mkataba wake kwa sasa.

HABARI ZA MICHEZO

4/8/2025

Kocha raia wa Afrika Kusini, Rulani Mokwena, ataendelea kukinoa kikosi cha Wydad Casablanca baada ya kikao kizito kufanyika kati yake na Rais wa klabu hiyo, Hicham Ait Menna, ambapo mustakabali wake katika kikosi hicho ulikuwa kwenye mizani.

Licha ya presha kubwa kutoka kwa wadau wa klabu wakitaka kocha huyo aondolewe kufuatia matokeo yasiyoridhisha, uongozi umeamua kuendeleza mkataba wake kwa sasa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo ya Morocco, gharama za kuvunja mkataba wa Mokwena ni kubwa mno – na kwa sasa, Wydad haina uwezo wa kifedha kugharamia hatua hiyo. Hili limekuwa mojawapo ya sababu kuu za kuendelea kwake, lakini pia kocha huyo amesisitiza wazi kuwa hana mpango wa kujiuzulu au kuondoka kwa hiari.

Mokwena, ambaye ameonyesha kujitolea na mapenzi kwa Wydad tangu alipowasili, amesema dhamira yake ni kuhakikisha anairudisha klabu hiyo kwenye mstari, akilenga kumaliza ligi katika nafasi ya pili ili kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao. Ingawa ndoto ya kushinda taji la ndani msimu huu imeyeyuka na pia baada ya kutupwa nje ya Kombe la Throne, nafasi ya kufuzu Klabu Bingwa Afrika bado iko mezani.

Kocha huyo mwenye falsafa ya kisasa ya mchezo anatarajia kutumia michezo iliyosalia kurejesha heshima ya Wydad na kuwapa mashabiki sababu ya kutabasamu.

Taarifa kutoka kwa watu wa karibu na klabu zinasema kuwa Mokwena hajaonyesha nia yoyote ya kuzungumza na vilabu vingine kwa sasa, kwani akili na moyo wake wote umeelekezwa kwa Wydad.

“Naipenda Wydad, na nina ndoto ya kuipeleka klabu hii kwenye Kombe la Dunia la Vilabu mwezi Juni,” amesema Mokwena kwa msisitizo.

Kwa sasa, sura mpya imefunguliwa kwenye ukurasa wa kocha huyo pamoja na Wydad, huku mashabiki wakiweka matumaini yao kwa mkufunzi huyo kijana lakini mwenye maono makubwa. Mechi inayofuata itakuwa muhimu si tu kwa sababu ya pointi za uwanjani, bali kwa uhusiano kati ya kocha na mashabiki – na huenda ikawa mwanzo wa kurejesha imani ndani ya Wydad Casablanca.