Khalid Aucho Kuwa Nje ya Uwanja kwa Wiki Tatu

Licha ya pengo litakaloachwa na Aucho, Yanga ina wachezaji wengine wenye uwezo wa kuziba nafasi hiyo.

HABARI ZA MICHEZO

4/9/2025

Klabu ya Yanga imepokea habari mbaya baada ya kiungo wake mahiri, Khalid Aucho, kuthibitishwa kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha takribani wiki tatu kufuatia jeraha la nyama za paja alilopata katika mechi dhidi ya Coastal Union.

Katika mchezo huo uliochezwa juzi, Yanga ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0, lakini furaha yao ilipungua baada ya Aucho kulazimika kutoka nje ya uwanja baada ya dakika 45 za kwanza kutokana na maumivu aliyohisi.

Taarifa rasmi iliyotolewa na klabu ya Yanga leo (jana) imeeleza kuwa vipimo vya kitabibu vimebaini jeraha hilo litamuweka Aucho nje ya dimba kwa takribani wiki tatu. Hii inamaanisha kuwa kiungo huyo atakosa michezo muhimu inayokuja, ikiwemo dhidi ya Azam FC itakayochezwa keshokutwa, Aprili 10, mchezo wa ugenini dhidi ya Fountain Gate mnamo Aprili 20, na mechi ya nyumbani dhidi ya Namungo FC kutoka Lindi, itakayopigwa Mei 13.

Licha ya pengo litakaloachwa na Aucho, Yanga ina wachezaji wengine wenye uwezo wa kuziba nafasi hiyo. Kocha anaweza kumtegemea Mudathir Yahya, ambaye tayari alichukua nafasi ya Aucho katika mechi dhidi ya Coastal Union, pamoja na Duke Abuya, Jonas Mkude, au Aziz Adambwile, kuhakikisha safu ya kiungo inasalia imara katika michezo inayofuata.

Mashabiki wa Yanga wanatarajia kiungo huyo apate uponaji wa haraka kwa Aucho ili arejee uwanjani kusaidia timu katika harakati zake za kusaka mafanikio ya klabu yake msimu huu. Wakati huo huo, benchi la ufundi lina kazi ya kuhakikisha mbinu sahihi zinatumika ili kuziba pengo hilo na kuendelea kupata matokeo mazuri katika michezo ijayo.