Coastal Union Wamfuta Kazi Mwambusi

Nimeijenga timu, lakini katika ushambuliaji kukawa na tatizo, hali hii imefanya tukose mtiririko wa matokeo mazuri.

HABARI ZA MICHEZO

4/7/2025

Coastal Union imetangaza kwamba kocha wao, Juma Mwambusi, ameachana na timu hiyo kwa makubaliano maalumu. Uamuzi huu umefikiwa siku moja kabla ya mechi yao inayopangwa kuchezwa leo Jumatatu dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam.

Mwambusi ambaye alijiunga na Coastal Union mnamo Oktoba 23, 2024 baada ya kuchukua mikoba ya David Ouma, ameiongoza Coastal katika mechi 15 za Ligi Kuu Bara ambapo katika kipindi chote timu hiyo imepata ushindi mara tatu, sare saba, na kupoteza mara tano hivyo kukusanya pointi 25 katika mechi 24 za msimu huu.

Taarifa za ndani kutoka Coastal Union zinasema kuwa uamuzi wa kumtimua Mwambusi umetokana na matokeo mabaya tangu alipoanza kuiongoza timu hiyo. Mwenyekiti wa klabu, Muhsin Ramadhan Hassan, alithibitisha taarifa hizi na kusema kuwa Mwambusi alitumwa Tanga kwa ajili ya kujadili hatma yake na mambo mengine ya kikosi.

Aidha, Katibu Mkuu wa Coastal Union, Omar Ayoub, alieleza kuwa yupo kikaoni na hakuweza kutoa maelezo zaidi kuhusu jambo hili, akisisitiza kuwa uamuzi huo ni wa makubaliano maalumu.

Kwa upande wa Coastal Union, hatua hii inatarajiwa kuleta mabadiliko muhimu katika utendaji wa timu, hasa kabla ya mechi dhidi ya Yanga.

Akizungumzia suala hilo Mwambusi amesema, "Sio tetesi ni kweli nimeondoka Coastal Union na kuanzia kesho (leo) hutoniona katika benchi katika mechi na Yanga SC. Nimeijenga timu, lakini katika ushambuliaji kukawa na tatizo, hali hii imefanya tukose mtiririko wa matokeo mazuri. Hakuna mgogoro katika benchi wala sijagombana na mwenzangu pale benchi, binafsi napenda kusimamia misingi ya kazi yangu"

Mpaka sasa, suala lisiloeleweka bado ni jinsi mabadiliko haya yatakavyoathiri utendaji wa Coastal Union katika mechi zijazo kuanzia na dhidi ya Yanga, lakini wapenzi wa soka wanatazamia mwanzo mpya yatakayojitokeza kutoka kwa klabu hiyo.